About Me

Friday, 4 September 2015

FRIDAY, SEPTEMBER 4, 2015

Saratani inavyoenezwa kwa samaki waliokaushwa kwa moshi wa plastiki



Samaki waliokaushwa.
Samaki waliokaushwa. 
By Clifford Majani
Njia za jadi za kuhifadhi samaki na nyama kwa muda mrefu ni kukausha kwa moshi. Ingawa kwa sasa dunia imepiga hatua kubwa katika teknolojia ya kuhifadhi vyakula kwa njia za kisasa kama vile matumizi ya majokofu na usindikaji, baadhi ya watu hasa katika maeneo ya vijijini bado wanatumia njia ya kuhifadhi samaki na nyama kwa kuzikausha kwa kutumia moshi.
Samaki waliokaushwa kwa moshi wanapatikana kwa urahisi katika masoko mengi ya vyakula katika vijiji, miji na majiji ya Tanzania. Jambo ambalo hatuna uhakika nalo kuhusu samaki hao, ni aina ya mali ghafi zinazotumiwa wakati wa kukausha samaki hao.
Upo uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya samaki hawa wanakaushwa kwa njia zisizozingatia na kujali afya ya walaji. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, sehemu nyingi zinakabiliwa na upungufu wa miti, kuni pamoja na mkaa. Na kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wanaamua kutumia nishati mbadala ikiwa ni pamoja na mabaki ya mifuko ya plastiki katika shughuli za upishi na uhifadhi wa chakula.
Vyombo kadhaa vya habari viliripoti mwaka jana kuwa baadhi ya maeneo katika Kanda ya Ziwa, samaki wanakaushwa kwa moshi wa mabaki ya vitu mbalimbali kama vile mbao, nguo kuukuu, pumba za mazao, karatasi, matairi na mifuko ya plastiki.
Hii inatokana na ukweli kuwa malighafi hizi zinapatikana bure au kwa gharama nafuu katika maeneo ambako samaki wanavuliwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waadilifu na wanaotaka kupata faida kubwa, wanaweza kushawishika na kutumia malighafi hizo kukaushia samaki bila kujali au kujua athari zake kwa afya ya walaji.
Matumizi ya malighafi hizi huongezeka sana wakati wa masika, kipindi ambacho kuni huadimika au kunyeshewa na kushindwa kutoa moshi wa kutosha kukaushia samaki.
Tafiti nyingi za masuala ya afya ya jamii, zinabainisha kuwa plastiki nyingi zinapochomwa huzalisha aina mbalimbali za sumu kama vile dioxin, furans, carbon monoxide, aldehydes na polynuclear aromatic hydrocarbons (PAH).
Moja ya tafiti hizo ni utafiti wa A. Valavanidid na wenzake uliochapishwa mwaka 2008 katika Jarida la Malighafi Hatari kwa Afya (Journal of Hazardous Materials) toleo la 156.
Utafiti wa A. R. Tricker na R. Preussmann nao unabainisha kuwa sumu ya nitrosamines ambayo ni moja ya visababishi vya saratani, hupatikana katika vyakula vilivyoandaliwa na kuhifadhiwa kwa moshi. Hii ni kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliochapishwa katika jarida la Mutation Research toleo la 259.
“Moshi unaotokana na chanzo cha polycyclic aromatic hydrocarbons umebainika kuwa na kemikali zinazochafua chakula na kukifanya kiwe na sumu ambayo tafiti zinaonyesha inachochea kuundwa kwa seli za saratani. Tafiti za kiepidemiolojia zinaonyesha kuwapo kwa uhusiano wa kitakwimu kati ya ongezeko la kutokea kwa saratani za njia ya chakula na utumiaji wa vyakula vilivyokaushwa kwa moshi,” inasema sehemu ya ripoti ya utafiti wa W. Fritz na K. Soós uliochapishwa mwaka 1980 katika jarida la kisayansi lijulikanalo kwa jina la Bibliotheca Nutrietio et Dieta, toleo la 29. Kwa kutambua hatari za kiafya zinazotokana na sumu za moshi wa mabaki ya plastiki, Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), wanajaribu kuhakikisha kuwa makubaliano ya Stockholm ya mwaka 2001 ya kupunguza uzalishaji wa moshi wenye sumu ikiwa ni pamoja na dioxin, yanatekelezwa katika nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Jamii haina budi kuchukua tahadhari kuhusu samaki waliokaushwa kwa moshi hasa pale wanapobaini au kuhisi harufu ya matairi, mifuko ya plastiki au harufu yoyote isiyopendeza kwenye kitoweo hicho. Mamlaka zinazohusika na usalama wa chakula kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Idara ya Udhibiti wa Ubora wa Samaki katika Wizara ya Uvuvi, hazina budi kuwa macho na kuwaelimisha wananchi kuhusu athari za kukausha samaki kwa malighafi zisizofaa kwa afya ya binadamu. Saratani ni moja ya magonjwa yanayoisumbua sana fani ya tiba kutokana na kuwa na mikanganyiko mingi katika kuitibu.
Saratani ni ugonjwa unaotokea baada ya kuwapo mparajikoano wa taarifa kwenye chembe za urithi ambazo hudhibiti mwenendo wa kuzaliana kwa seli katika organi fulani ili kuendelea kuifanya itende kazi kwa usahihi.
Mparajikano huo husababisha seli zisizo za kawaida kuzaliana na kuongezeka idadi pasipo kudhibitiwa hivyo kuifanya organi au viungo viwe na umbo tofauti na ilivyo kawaida.
Hali hiyo ya kuzaliana bila utaratibu inaweza kusababisha athari kuvamia sehemu nyingine za mwili na kuleta madhara. Saratani huweza kusambaa maeneo mengine ya mwili.
Taasisi ya Saratani ya Ocean Roard (ORCI), inasema kuwa idadi ya wagonjwa wapya wa saratani wanaofika kutibiwa inaongezeka kwa kasi toka wagonjwa 2,807 mwaka 2006 hadi kufikia 5,529 mwaka 2013. Dk Julius Mwaiselage wa ORCI anasema ongezeko kubwa la maradhi haya hapa nchini linatokana na mfumo wa maisha ya Watanzania kwa sasa.
Kauli ya Dk Mwaiselaga inaungwa mkono na ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2010, ilibainika kuwa miongoni mwa sababu za ongezeko la saratani hapa nchini ni pamoja na mtindo wa maisha usiofaa.

Maoni au maswali tuma afya@mwananchi.co.tz au 0713247889

No comments:

Post a Comment